3 Septemba 2025 - 23:40
Source: Parstoday
UN: Israel imewadondoshea maguruneti askari wetu wa kulinda amani Lebanon

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani nchini Lebanon (UNIFIL) kimesema kuwa ndege zisizo na rubani za Israel zilidondosha maguruneti manne karibu na kambi ya walinda amani waliokuwa wakifanya kazi ya kuondoa vizuizi vya barabarani Jumanne asubuhi.

"Hili ni moja ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya wafanyakazi wa UNIFIL na mali zake tangu kusitishwa kwa makubaliano ya uhasama mnamo Novemba mwaka jana," UNIFIL ilisema katika taarifa yake Jumatano.

Guruneti moja lilianguka ndani ya mita 20 na tatu ndani ya takriban mita 100 karibu na wafanyakazi na magari ya Umoja wa Mataifa. UNIFIL ilisema kuwa wanajeshi wa Israel walikuwa wamefahamishwa mapema kuhusu kazi ya UNIFIL ya kusafisha barabara katika eneo hilo, kusini mashariki mwa kijiji cha Marwahin.

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza kwa kauli moja muda wa ujumbe huo wa kulinda amani nchini Lebanon hadi mwisho wa 2026, ambapo baada ya mwaka mzima uondoaji wa utaratibu wa askari hao wa mwaka mzima utaanza. Ilianzishwa mwaka 1978, UNIFIL inalinda mpaka wa kusini wa Lebanon na Israel.

Hii ni katika hali ambayo, mwanzoni mwa mwaka huu, viongozi wa Lebanon waliwataka waangalizi wa kimataifa wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel kuulazimisha utawala huo wa Kizayuni uondoe kikamilifu vikosi vyake kusini mwa Lebanon kabla ya mwisho wa Januari, 2025.

Hata hivyo, jeshi la utawala huo wa Kizayuni limeendelea kubaki ndani ya ardhi ya Lebanon, bali hata linaendeleza mashambulizi ya kikatili ya mara kwa mara ya viongozi na hata raia wasio na hatia wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNIFIL) mara kwa mara kimetaka kuondoka kikamilifu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa Lebanon.

Umoja wa Mataifa mara kadhaa umeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, kuwashambulia walinda amani wa umoja huo kunakiuka sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba ukiukaji huo unaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Your Comment

You are replying to: .
captcha